SOMO LA KWANZA
"Simama upate kubatizwa na kufutiwa dhambi zako, ukilita jina la Bwana."
Somo katika kitabu cha Matendo ya Mitume 22:3-16
Siku zile: Paulo aliwaambia watu [huko Yerusalemu], "Mimi ni
Myahudi, mzaliwa wa Tarso katika Silisia, lakini nililelewa katika
mji huu huu. Nilikaa miguuni pa Gamalieli na kuelimishwa barabara
kadiri ya Sheria za baba zetu na nikawa mpenzi wa Mungu, kama
ninyi nyote mlivyo leo. Kwa hiyo niliwatesa wafuasi wa Njia hii,
nikawa tayari kuwaua, niliwafunga wanaume kwa wanawake na
kuwatia gerezani.
Kuhani mkuu na halmashauri yote ya wazee waweza kushuhudia
mambo hayo. Kwao nilipata barua kwa ndugu, nikaenda Damasko,
ili huko pia niwafunge wafuasi wa Njia mpya na kuwapeleka
Yerusalemu wapate kuadhibiwa.
Lakini njiani nilipokaribia Damasko, ilitukia wakati wa adhuhuri
kwamba mwanga mwangavu ulitoka ghafula mbinguni, ukaniangazia pande zote. Nikaanguka chini na kusikia sauti ikiniambia,
'Sauli, Sauli, mbona unanitesa?" Nami nikajibu, U nani, Bwana?"
Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti ambaye wewe unanitesa."
Wenzangu waliuona mwanga lakini hawakuisikia sauti ya yule
aliyesema nami. Nikauliza, 'Bwana, nifanye nini?
Bwana akaniambia, Simama, uingie Damasko, huko utaambiwa
yakupasayo kufanya."Kwa kuwa nilishindwa kuona kitu kwa sababu ya mng'aro wa
mwanga ule, wenzangu walinishika mkono na kuniongoza, na hivyo
nikaingia Damasko.
Mtu fulani, kwa jina Anania, mcha Mungu na mshika Sheria,
mwenye sifa njema kwa Wayahudi wote waliokaa huko, alikuja
kwangu, akasimama mbele yangu, akaniambia, Ndugu Sauli,
ona tena.' Mara nikaona. Naye akaniambia, Mungu wa baba zetu
amekuchagua upate kutambua atakalo yeye, kumwona Mwadilifu
na kusikia sauti itokayo kinywani mwake; kwa maana utakuwa
shahidi wake kwa watu wote katika hayo uliyoyaona na kuyasikia.
Na sasa, unakawia nini? Simama upate kubatizwa na kufutiwa
dhambi zako, ukilita jina lake. '"
Neno la Bwana.
AU SOMO LIFUATALO:
SOMO LA KWANZA
"Utaambiwa yakupasayo kufanya."
Somo katika kitabu cha Matendo ya Mitume 9:1-22
Siku zile: Sauli alikuwa amenuia kuwatesa wafuasi wa Bwana,
akatishia kuwaua, akaenda kwa kuhani mkuu, akaomba barua
kwa ajili ya masinagogi ya Damasko, ili, akiwakuta huko wafuasi wa
Njia hii awafunge, waume kwa wake, na kuwaleta Yerusalemu.
Lakini njiani, alipokaribia Damasko, ilitukia kwamba ghafula
mwanga kutoka mbinguni ulimwangaza pande zote. Akaanguka
chini na kusikia sauti ikimwambia. Sauli, Sauli, mbona unanitesa?"
Akauliza, "U nani, Bwana?"Naye akajibu, "Mimi ni Yesu unayenitesa.
Lakini simama, ingiamjini na huko utaambiwa yakupasayo kufanya." Wasafiri wenzake
walisimama wakishangaa, maana walisikia sauti, lakini hawakumwona mtu.
Sauli akainuka toka chini, lakini alipofumbuamacho hakuona kitu; basi,
wakamshika mkono, wakampeleka mjini
Damasko. Siku tatu alikuwa kipofu. hakula wala hakunywa.
Huko Damasko kulikuwa na mfuasi. jina lake Anania, na Bwana
akamwita katika njozi, "Anania." Naye akajibu, "Nipo, Bwana." Bwana akamwambia, "Simama uende katika barabara iitwayo Nyofu na huko katika nyumba ya Yuda umtafute mtu aitwaye Sauli
wa Tarso, yupo kule anasali, naye katika njozi amemwona mtu jina
lake Anania, akiingia na kumwekea mikono apate kuona tena."
Lakini Anania akajibu, "Bwana, kwa watu wengi nimesikia habari
za mtu huyu na mabaya kiasi gani aliyowatenda watakatifu wako
huko Yerusalemu. Hata hapa ana mamlaka kutoka kwa makahuni
wakuu kuwafunga watu wanaoliita jina lako." Lakini Bwana
akamwambia, "Nenda, kwa maana mtu huyu ni chombo kiteule
kwangu achukue jina langu kwa mataifa, na wafalme na Waisraeli,
na nitamwonyesha ni mambo gani atapaswa kuteseka kwa ajili ya
jina langu." Anania akaenda, akaingia nyumba ile; akamwekea mikono
akisema, "Ndugu Sauli, Bwana Yesu aliyekutokea njiani ulipokuwa
unakuja, amenituma upate kuona tena na kujazwa Roho Mtakatifu."
Mara hapo machoni, madude kama magamba yakabanduka, akaona
tena. Akasimama na akabatizwa. Na baada ya kula, nguvu zake
zikamrudia.
Siku chache akikaa na wafuasi wa Damasko, mara akaanza kuhubiri
habari za Yesu katika masinagogi, akisema, “Yeye ni Mwana wa
Mungu." Wote waliomsikia walishangaa, wakasema, Je, si huyu
aliyewaangamiza wenye kuliita jina hili huko Yerusalemu? Na
hakuja hapa kusudi awafunge watu hawa na kuwapeleka kwa
makuhani wakuu?" Sauli akaimarika zaidi na zaidi,
akawahangaisha Wayahudi wa Damasko, akithibitisha,
"Huyu ni Masiya."
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 117:1, 2 (K. Marko 16:15)
K. Nendeni duniani kote, mkaihubiri Injili.
au: Aleluya.
Msifuni Bwana, enyi mataifa yote!
Mtukuzeni Bwana, enyi watu wote! K.
Maana wema wake kwetu sisi ni mkuu,
na uaminifu wa Bwana ni wa milele. K.
SHANGILIO LA INJILI
Tazama Yohane 15:16
Aleluya.
Mimi niliwachagua ninyi, ili mwende kuzaa matunda, na matunda yenu yadumu, asema Bwana.
Aleluya.
INJILI
"Nendeni duniani kote, mkaihubiri Injili."
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko 16:15-18
Wakati ule: [Yesu aliwatokea wale kumi na mmoja], akawaambia,
"Nendeni duniani kote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.
Atakayeamini na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.
Ishara hizi zitafuatana na waumini: kwa jina langu watatoa pepo
wabaya, watasema lugha mpya. Watashika nyoka, hata wakinywa
sumu ya kuua, haitawadhuru.
Wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapona."
Injili ya Bwana